Wednesday, July 2, 2008

Naombeni Radhi Masela! Profesor J


Naombeni Radhi Masela!
Msanii na mmoja wa waasisi nguli wa muziki wa Hiphop nchini,Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay au Big Daddy kama anavyojulikana na wengine, amewaomba radhi baadhi ya wasanii na wanamuziki wenzake wote, ambao kwa namna moja au nyingine amewahi kuwakosea kwenye shughuli zao za kimuziki.
Prof Jay aliomba radhi hiyo kupitia kipindi cha ‘Hip-Hop Base’ kinachorushwa na Luninga la Channel 5 wiki iliyopita, wakati akijibu swali la mwongozaji wa kipindi hicho, kuhusu malalamiko yanayotolewa na wasanii kadhaa dhidi yake, kuwa huwaringia wanapomwomba kumshirikisha katika track zao. “Ni kweli nimewahi kuitwa na wasanii kadhaa katika shughuli zao, lakini nilishindwa kuhudhuria - wakati mwingine mchakamchaka ndiyo unaonifanya nishindwe kwenda, sikukataa kwa makusudi, huwa napenda nikishirikishwa niwe nimejiandaa vilivyo, naomba waniwie radhi wote niliowakosea,” alisema Profesa Jay. Mwanamuziki huyo ambaye amepata tuzo mbalimbali ikiwamo ya utawala bora, aliyoipata kutokana na albamu yake ya ‘Ndiyo Mzee’ ambayo ilitolewa na Redio One na BBC, aliwataka wasanii na wanamuziki wenzake nchini, kudumisha ushirikiano ili kukuza muziki wao. Aliisifu tuzo hiyo ya Utawala Bora, aliyoipata pamoja na viongozi wengine kadhaa mahiri, akiwamo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Joseph Warioba, na kusema kuwa ilimpa sifa lukuki. Pamoja na mambo mengine, alisema huchukua muda mrefu kutoa albamu, ili aweze kutoa kitu cha uhakika. “Albamu kwangu ni kama nembo, ndo maana huwa natoa albamu baada ya miaka miwili,” alisema mwanamuziki huyo, ambaye albamu zake nyingine ni ‘Jina langu’, ‘Mapinduzi halisi’ na ‘Machozi ya damu’.

No comments: